Friday, June 29, 2007

MAMBO YA VIVULI


Huyu ni Rokia Traore, mwanamuziki toka Mali, na bendi yake. Walikuwa wakitumbuiza kwenye mkutano wa TEDGlobal pale Arusha. Sasa wakati watu wote walielekeza macho yao kwenye jukwaa, kamera yangu ikaking'amua kivuli hiki kwenye ukuta, pembeni kidogo ya jukwaa. Picha hii nimeichezea kidogo kwenye Photoshop.

NOTIS


Usicheze na wenye nyumba bwana. Ukikaanga sana kuliko yeye huchelewi kurudi siku moja ukakuta mambo kama haya. Wapangaji take care.

SELO


Uko msemo wa kiingereza usemao "Even Freedom is not Free, It has a Price Tag". Usijedhani picha hii niliipigia jela, lahasha, hiki ni kivuli cha dirisha la ofisi yangu. Nilipoona kivuli hiki kwenye sakafu nikakifananisha na mlango wa selo.

UPWEKE


Kuna siku mtu unaweza ukaamka usijue unatakiwa kufanya nini. Hii ilinikuta siku ya Jumamosi ya tarehe 23/6/2007. Basi nikazama jikoni na kujitengenezea kikombe cha chai ili kupitisha muda. Basi wakati nimekiweka kikombe hiki mezani huku nikiendelea kuwaza na kuwazua nifanye kitu gani jumamosi ile nikavutiwa na upweke wa kikombe hiki cha chai ya mkono mmoja. Fasta nikaiwahi kamera yangu na kubaruza foto hii.

Friday, June 22, 2007

MUNGU HULALA AFRIKA


Jana baada ya kukaa kwenye tarakilishi kwa masaa yasiyopungua kumi nikaamua kwenda ufukweni kusafisha macho, kama kawaida huwa sitoki bila SONY DSC-P32 mfukoni. Ni kamera ndogo na huwa nikiitoa mbele za watu wananicheka.


Sasa jana kwenye kutembea kwangu pembezoni mwa ufukwe wa Msasani (karibu na Sleepway) nikauona mwale wa jua uliochagua mmoja ya mitumbwi iliyokuwa imetulia baharini. Sijui nilifikiri nini, ila niliamini kuwa mwale ule una mahusiano na Mungu na pengine ni Mungu amemchagua mvuvi mwenye kumiliki mtumbwi ule ili ajisitiri kwa usiku ule. Sounds Crazy unhhh?!


Mungu hulala Afrika na pote pengine. Tafadhali tembelea picha zangu zaidi katika http://www.flickr.com/ , kule utanipata kwa jina la “babukadja”. Picha hii kwa kule nimeiita “God Sleeps in Africa”

Wednesday, June 20, 2007

NITAFUTE WWW.MWENYEMACHO.WORDPRESS.COM

Ndugu msomaji wa blogu hii, utaniwia radhi kwa usumbufu ila sina budi kukusumbua japo ni kwa starehe yetu sote kwa baadae.

Nimepewa ushauri na wakongwe wa fani ya kublogu kuwa kublogu kwenye mfumo wa WORDPRESS kuna raha zaidi kwa yule anayeblogu na kwa wateja wa blogu hiyo pia. Nimeijaribu WORDPRESS na kwa kweli ina mvuto wa aina yake.

Tafadhali kuanzia muda huu naomba unitafute katika http://www.mwenyemacho.wordpress.com/ .

Samahani na karibu http://www.mwenyemacho.wordpress.com/ , yote kwa wakati mmoja

Monday, June 18, 2007

ATI HII NI HAKI?

Jana majira ya jioni nilitoka kidogo kwenda kupata bilauri ya mvinyo na rafiki yangu mmoja anaitwa Sarah, jina la pili sitakupati kwa sasa, yeye ni mwandishi wa habari toka shirika la habari la Reuters (Hebu cheki vizuri, nimepatia speling?). Sasa katika blablaa zetu akanipa moja kali.

Ilikuwa siku ya Alhamisi iliyopita, alisafiri na ndege ya Precision Air akitokea Kilimanjaro kuja Dar es Salaam kupitia Zanzibar. Sasa kwenye ndege akaona ile inflight magazine ya ndege hiyo. Sarah anapenda kutengeneza pesa kwa kazi yake ya uandishi, hivyo alipofika pale Mwalimu Nyerere Airport fasta akakimbilia kwenye ofisi za hawa jamaa. Kufika pale jamaa wa pale ofisini full kumchangamkia Sarah, mzungu tena! (ndio Sarah ni Mmarekani)

Basi Sarah akaomba kuonana au kuongea na afsa mhusika, jamaa fasta wakamuunganisha kwenye simu. Sarah alikuwa anataka kujua yeye kama muandishi anaweza kuchangia makala kwenye magazine ya Precision Air. Afsa mhusika akamjibu kuwa anakaribishwa kwa mikono miwili, tena wana uhaba mkubwa wa wachangiaji (yani waandishi)

Sarah kusikia vile tabasamu likamjaa usoni, wale jamaa pale ofisini wakadhani anawatabasamia wao nao wakatengeneza tabasamu, kumbe mwenzao anafurahia opportunity. Sarah akajua hapa atatengeneza pesa ya kununulia mvinyo Dar.

Basi Sarah akaenda mbele zaidi, akamuuliza Afsa mhusika, "Enhe, huwa mnalipa shilingi ngapi kwa makala?" Afsa mhusika fasta akampa, "Huwa tunalipa kwa kila neno unaloandika...". Rafiki yangu Sarah akaona kweli dunia imekuwa tambarare 'yani hata Tanzania wanalipa kama Reuters!' (cheki tena speling aisee). Sarah kikamtoka kicheko kwa nguvu, wale jamaa pale ofisini nao wakaachia kicheko cha nguvu, sijui Sarah ana kicheko cha kuambukiza maana jamaa walikuwa hata hawajui mwenzao anacheka nini.

Basi Sarah akampa Afsa mhusika, "I think we can do business". Afsa mhusika nayeye akampa, "Definetly". Sarah akauliza, "Kwa hiyo mnalipa shilingi ngapi kwa kila neno moja la makala?", Afsa mhusika akampa, "Six to Ten Shillings". Sarah akapigwa na butwa asijue la kufanya, basi taratibu akarudisha kisemeo kwenye simu na taratibu akaanza kuondoka bila kuaga.

Sasa jana wakati ananipa kisa hiki akaniambia aliondoka bila kuaga si kwa kupenda bali kichwani alikuwa anajaribu kupiga hesabu kuwa makala yenye maneno miasita ingemlipa pesa ngapi, jibu likaja elfu sita. By the time anapata jibu alishawapita wale jamaa pale ofisini hivyo hakuwaaga.

Sasa hiyo elfu sita ambayo angelipwa ingemtosha kununua glasi mbili tu za huo mvinyo aliokuwa anakunywa na magazine inatoka mara moja kila mwezi. Sarah akaishia kuniuliza, "Bob, ati hii ni haki?". Sikuwa na jibu, labda wasomaji wa blogu hii mumsaidie.

Friday, June 15, 2007

KAZI NA DAWA

Hivi niliwahi kukuambia kuwa ninafanya kibarua na jamaa fulani wanajiita MEDIA FOR DEVELOPMENT INTERNATIONAL? Kama hapana basi hapo ndipo nilipo, na picha hii nimeipiga majira ya saa kumi kasorobo jioni ya leo. Nilivutiwa na jua lilikuwa linagonga hapo kwenye meza

Huyu aliyemo katika picha hii ni rafiki yangu anaitwa Paul Ndunguru au Baba Paka (Kwa ufafanuzi zaidi kuhusu hilo jina la pili muulize Ndesanjo Macha wa http://www.jikomboe.com/. Jamaa ni mchoraji wa katuni na mazagazaga mengine. Atakuwa na blogu hivi karibuni, umtembelee tafadhali. Hapa jamaa anapiga kazi huku anapata kababu na machicha ya nazi. Kazi na dawa bwana.


Picha hii pia niemiweka kwenye mtandao wa http://www.flickr.com/, tafadhali tembelea mtandao huu uone kazi za wapiga picha wengine. Huwa napata ideas nyingi sana humu.


Kuna kitu nimegundua baada ya kupiga picha hii, nadhani picha za Black and White bomba sana. Unaonaje nikiendelea kukuletea picha za mtindo huu hapa bloguni? Pale inapobidi tulete za rangi tutafanya hivyo. Naomba maoni

UHURU NA VIDEO MKUNJUO

Nimetembelea blogu inaitwa http://www.onlinejournalismblog.wordpress.com/ nikakutana na habari hii "THE VIDEO JOURNALIST NEXT PURCHASE", Nikaona si vibaya nikiitafsiri kwa ndugu zangu wote wanaopenda teknolojia digitali, kublogu, pamoja na kiswahili.

Jamaa wanajiita Pure Digital Technologies, wametengeneza kajikamera haka kakurekodia picha za video na kuzirusha kwenye blogu yako kwa urahisi wa kupindukia. Wameipa jina la Flip Video (Video Mkunjuo). Jamaa wanadai kuwa wanataka swala la kublogu kwa picha na video lisiwe jambo la kutisha kiasi kwamba ukate tamaa na kuwaachia kazi hiyo watu kama kaka Issa Michuzi, au rafiki zangu Mjengwa na Mroki au Mwenye Macho.

Jamaa wa Pure Digital Technologies wanasema ni jukumu lao kuhakikisha kuwa wanatengeneza chombo hiki ili upashanaji wa habari za kiraia kwa njia ya video uwe rahisi na wa haraka kabisa. Kwa mawazo yangu ukiwa na hii kitu utaweza kuwatoa umaarufu CNN, ITV, BBC, FOX TV na wengine kama hao. Yani unaanzisha TV yako, kwa mfano Mwenye Macho TV.

Kamera hii inalingana na simu yako ya mkononi na inakuwezesha kukamata matukio bila kusumbuliwa na 'dola' wakati mwingine. Kwa mfano unaweza kurekodi jinsi askari wa jiji la Dar es Salaam wanavyokamata vyakula vya kina mama ntilie na kuvila wao wenyewe badala ya kuvipeleka vinakohusika. Jamaa wanaiuza kwa dola za kimarekani $129.99(bei ya kimatangazo hii) kwa maana nyingine ni $130.
Inasemekana kuwa hii ni kamera ya kwanza inayomwezesha mpiga video kuipiga video, kuihariri na haitamaye kuirusha video kwenye blogu bila kupoteza muda mwingi kwenye tarakilishi yako.

Wito wangu kwa wanablogu wa Tanzania, wapendao kublogu kwa picha na video, ni kuwa yatubidi kufanya mpango wa kupata hii kitu na kuanza kupashana habari kwa Waswahili waliomo ndani na nje ya nchi.

Monday, June 11, 2007

HONGERA SUMAYE LAKINI...!

Basi tangu nimetoka kwenye mkutano wa TED nimekuwa na mambo kadhaa yananikimbiza mchakamchaka hadi muda wa kublog unataka kuniponyoka. Lakini nimejiwekea nadhiri kuwa japo mara moja kwa wiki lazima nipandishe kitu hapa.

Sasa leo katika upekuzi wangu nikagonga hodi www.mjengwa.blogspot.com. Ile kukaribishwa tu nikakutana na picha hii. Sikuwa na lazaidi la kusema zaidi ya kumpongeza Sumaye.


Lakini wakati huohuo nikaanza kuwaza, unajua jamaa alipokuwa Waziri "Mkubwa" tulikuwa tunampa heshima kama Mungu. Kwa mfano tulikuwa tukitaka kumwambia jambo lazima uanze na "Mheshimiwa Waziri 'Mkubwa'...", halafu ndio unaendelea na swala lako unalotaka kusema, labda, "Mheshimiwa Waziri 'Mkubwa', samahani naweza kukuvua viatu". Sasa nikawa najiuliza jamaa si atakuwa amepata tabu sana pale Havard maana huko nasikia walikuwa wanampita tu, wale wachache waliokuwa wanaomfahamu ndio labda walikuwa wakimwita kwa jina lake la kwanza, mfano, "Freddy ehh, unajua kesho ndio 'deadline' ya 'assignment', mbona jana hatukukuona kwenye 'discussion'?".


Mbili, jamaa alipokuwa kiongozi hapa yani hata hotuba ya karatasi mbili alikuwa anabebewa. Kula leki viongozi wa kibongo! Sasa huko sijui nani alikuwa anambebea majitabu yake, labda aliajiri mtu!


Tatu, niliposikia jamaa anakwenda kusomea uongozi nikapigwa na butwaa na maswali kibao yakajiri kichwani mwangu. Swali kubwa lilikuwa ni "Umetuongozaje kwa miaka kumi bila ya kuwa na ujuzi wa kuongoza?" Hata hivyo nikajifariji kuwa labda sasa baada ya kuhitimu Freddy atakuwa anajua kuwa kiongozi aliye bora sio tu habebewi hotuba, bali hata kuandikiwa ni mwiko, kwani mbebaji anaweza kupoteza baadhi ya kurasa na mwandishi huandika mawazo yake na siyo ya mtoa hotuba.


Sina la ziada zaidi ya kumpongeza aliyekuwa Waziri 'Mkubwa' wetu, HONGERA FREDDY!

Friday, June 8, 2007

TED IMEFIKA TAMATI

Mkutano uekwisha, ulikuwa murua. Hapa watu wameongeza marafiki, wameongeza anuani, wameongeza miradi ya kufanya mwaka huu.

www.mwenyemacho.blogspot.com imezaliwa pia na imepatiwa nyenzo ya kuifanya iwe bora zaidi, laptop (Mac Book Pro) ya bure toka Google. Pamoja na radio ya Satelite ambayo itaiwezesha Mwenye Macho kupata habari kadha wa kadha na kuzitupa kwenye blogu hii. Kaa mkao wa kula.

Wosia wangu kwa watanzania ni kuwa tujitahidi kuhudhuria semeina au workshop au mkutano japo mmoja kwa mwaka. Kwani huwezi kujua kuwa utakutana na nani na utafungua milango gani katika masha yako.

Nimesikitishwa na kitu kimoja, mkutano umefanyika Tanzania lakini waliopanda kutoa mada kwenye jukwaa la TED ni Watanzania wawili tu, Rais Kikwete na mjasiramali Ali Mufuruki.

Hata Watanzania waliohudhuria mkutano huu ni wa kuhesabu. Tujitahidi wakati mwingine na tuendelee kublogu kwa nguvu zote.

Naelekea nyumbani sasa. Nilikuja kwenye mkutano lakini nina kiporo niliacha. Natengeneza filamu iitwayo "Funguo" Itatoka muda sio mrefu. Endelea kufuatilia kurasa hizi ujue mustakabali wa mradi huu. Asante kwa kufuatili mkutano wa TED kupitia blogu hii na nyinginezo. Wakati mwingine...

YALIYOJIRI JANA

Najitayarisha kwenda uwanja wa ndege wa Kilimamanjaro tayari kurudi nyumbani. Lakini kuna vitu nilitakiwa kuvirusha jana ila muda ukabana. Naona haitakuwa vyema kuondoka bila kukupatia.

Jana jioni baada ya mapumziko mafupi, na chai ya jioni, kwenye jukwaa alipanda Chris Abani. Yeye ni Mwandishi wa vitabu na mshairi. Ababni ni Mnigeria kalini anakaa Marekani, ni profesa wa masuala ya fasihi katika chuo kikuu kule.

Abani ameandika mambo mengi ya kukosoa unyonyaji wa bara la Afrika na pia amekuwa mwiba mchungu kwa viongozi maharamia wa Nigeria na Afirka pia. Amewahi kufungwa jela mara tatu kwa sababu ya maandishi na mashairi yake yasiyo na sime kusema "MFALME YUKO UCHI!"

Abani amepanda kwenye jukwaa na anongelea jinsi teknolojia inavyomsaidi kuandika mambo ya nyumbani angali yu mbali. Anaongea mambo kadhaa tafadhali yasome kwa Ethan Zuckerman na Ndesanjo Macha.

Ababni anamaliza dakika zake arobaini na tano alizopewa kutoa mada, lakini hatuachi hivihivi anatuacha na Shairi. Anapomaliza ukumbi unalipuka kwa vigelegele na vifijo. Aisee huyu jamaa si mchezo.

Kabla hata hatujajiweka vyema kwenye viti vyetu, unapanda mwiba mwingine wa uandishi toka Kenya, huyu si mwingine bali Binyavanga Wainaina. Sitaki kukuficha, huyu jamaa sijawahi kumwelewa hata siku moja, huwa anaongea mambo mengi kwa wakati mmoja. Mara ya kwanza nilikutana naye Zanziba mwaka 2005, kwenye tamasha la filamu, akanizawadia insha yake iitwayo "How to Write About Africa". Ilinibidi kuisoma mara tatu kuweza kuelewa alichokuwa anasema.

Sasa leo tena amepanda hapa jukwaani na kutuambia tufunge macho. Halafu anaanza kusoma insha yake fulani hivi, kwa dakika mbili. Anapotuambia tufungue macho watu kadhaa wanapiga makofi ila nina hakika wengi wetu, mimi nikiwemo tunafuata mkumbo tu, hatujaelewa kitu. Binyavanga anatabasamu kwa sababu anajua ameshawakoroga watu, anashukuru na kuondoka zake. Soma zaidi kuhusu Binyavanga katika www.jikomboe.com

Baadae jukwaani anapanda Franco Sacchi, ni mtengeneza filamu na Prodyusa wa filamu ya This is Nollywood. Ni Muitaliano huyu jamaa lakini amezaliwa Zambia. Filamu yake ni dokyumentari inayoonyesha maendelea ya utengenezaji wa filamu wa Nigeria. Franco anatwambia kuwa Afrika ikipatiwa Teknolojia muafaka inaweza kwenda sambamba na sehemu zingine za ulimwengu na hili limethibitishwa na maendeeo ya haraka ya fani ya filamu katika Nigeri. Anasema kwa mwaka jana pekee, Nigeria imetengeneza filamu 2000. Nigeria ni nchi ya tatu kwa utengenezaji wa filamu ukiacha Marekani na India.

Franco ameambatana na muongozaji wa filamu za Kinigeria anaitwa Bon Emeruwa, bila ajizi baada ya Franco kumalaiza mada najivuta kukutana na Bond. Kujivuta huku si kwa ajili ya kupata picha tu, hapa ni biashara sasa. Ukumbuke kuwa mimi pia ni mtengeneza filamu. Naongea mambo kadhaa na Bond kama bajeti za filamu zake, anapiga picha kwa muda wa siku ngapi na anasambaza vipi filamu zake. Tunabadilishana anuani zetu, na tunapeana ahadi za kutembeleana na kusaidiana katika miradi ya filamu zetu. Na mwisho namuomba tupige picha ya ukumbusho. Nakuona unatasamu, ahahahahah!

Haya na mwisho kabisa anapanda yule gwiji la muziki toka Afrika ya kusini, yeye anaitwa Vusi Mahlasela. Vusi si mwanamuziki tu, ni mshairi, na alikuwa pia na bado ni wanaharakati dhidi ya ubaguzi wowote wanrangi.

Jamaa anapiga gita lake na kuimba mwenyewe, ila kama uko nje ya ukumbi huu unaweza kudhani kuna watu watatu au wanne kwenye jukwaa. Jamaa kuna namna anashirikiana na gitaa lake na kutoa saiti zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Naona hata Rokia na Abenaa wametulia kimya, bwana mkubwa yuko kazini. Usipime. Soma zaidi kwenye www.jikomboe.com

Hivyo ndivyo kamera yangu ilivyoishuhudia jana.

LEO NI KAMA KRISMAS

Ni muda wa mapumziko baada ya JK kutimka, watu wanapata chai ya saa nne asubuhi. Katika muda huu pia napata nafasi ya kukutana na rafiki yangu, mwanablogu, mwanzilishi wa Global Vioces, Ethan Zuckerman. Niliongea na Ethan jana akaniambia ameipenda sana blogu yangu na angependa kuona blogu nyingi zaidi za Kiswahili zikiibuka na yuko tayari kuzipa support. Watanzania tuandike kwa Kiswahili jamani, internet imepungukiwa lugha hii.

Nilisahau kukwambia kwamba leo asubuhi sisi washiriki miamoja tuliodhaminiwa na TED kuhudhuria mkutano huu, wakiwemo Watanzania kadhaa, tumezawadiwa laptops kila mmoja. Eti jamaa wanatuambia tuchague kati ya Mac au PC. Kula leki TED.

Samahani, sikufanikiwa kuwapiga watu picha walipokuwa wanashangilia kwani na mimi nilikuwa nashangilia pia. Ilikuwa nderemo na vifijo sio mchezo.

Pia kuna mtoa mada mwingine anaitwa Noah Samara, yeye ni mzakiwa wa Sudan lakini anaishi Marekani hivi sasa, yeye ndiye mwanzilishi na mmiliki wa radio ya WorldSpace. Yeye pia ameahidi wahudhuriaji 100 wakiwemo, Watanzania kadhaa, kwamba atawapatia radio hizo amabazo hupokea mawimbi yake toka kwenye satelait. Yani nitaweza kupata habari toka sehemu yeyote duniani, moja kwa moja. Ndio, hata Iraq pia!

Tafadhali soma zaidi habari hizi kwa Ethan (www.ethanzuckerman.com) na Ndesanjo (www.jikomboe.com)

Thursday, June 7, 2007

KILA KITU NI MUHIMU KWANGU - JK

Rais wangu, Kikwete ameshaingia kuufunga mkutano wa TED, dah! yani leo humu ndani hakuna amani kabisa, kumejaa jamaa wa usalama wa taifa kibao na si unajua kuwa wale jamaa huwa hawaruhusiwi kukaa, basi hata picha hatuzipati vizuri. Yani kila nikipata angle nzuri, jamaa kakatiza. Si mbaya lakini, hii ni kwa usalama wa rais wangu.

Sasa mheshimiwa rais anatoa hotuba, wakati anapanda kwenye jukwaa alikuwa amevaa suti yake safi sana. Lakini ili uwe mwanaTED mzuri, amri ya kwanza ni kutokuvaa suti, unatakiwa uvae kawaida ili uweze kufanya kazi. Basi raisi alipopanda tu jukwaani akijistukia kuwa amechemka, fasta akamwita mlinzi wake na kumkabidhi koti, watu full makofi. Ila naona kiongozi wa msafara amekasirika kwa sababu hata yeye amevaa suti, sasa anajishauri, je avue au abaki alivyo? Bosi wake amevua!

JK amenifuraisha kitu kimoja, anazungumzia maendeleo ya Teknolojia na Afrika. Anasema kila kona ya dunia anayokwenda huulizwa ni kitu gani anachotilia umuhimu katika maendeleo ya wananchi wake? Yeye huwajibu "Kila kitu". Hotuba yake ni fupi sana na amemaliza.

Sasa ni kipindi cha maswali, wanaTED wanamuuliza ni kitu gani kinamkera katika siasa za Afrika. Anajibu, "Nafadhaishwa na viongozi wa kijeshi wanaoamka asubuhi moja na kuteka radio na kutangaza serikali mpya isiyo ya kidemokrasia."

Anaulizwa, "Je wewe unajali demokrasia?", kama kawaida yake anatabasamu kwanza halafu anajibu kuwa anadhani anajali demokrasia. Jamaa anauliza unatumia kipimo gani kujua kuwa unajali demokrasia? Anasema, nguzo kubwa anayotumia kujipimia ni uhuru wa vyombo vya habari. Anasema kuna magazeti lukuki Tanzania, na hicho ni kitu kizuri kwani inasaidia kukosoa yule anayetenda kosa na ni jukumu la mkoslewaji kuelewa. Watu makofi wawawawawa!

Anaulizwa, unadhani misaada ni sumu kwa Afrika? Anasema yeye yuko tofauti kabisa na hilo, yeye anaamini kuwa misaada ni kitu safi sana ila itumike vizuri la sivyo itageuka kitanzi kwa mkopaji.

Anazungumzia rushwa Afrika. Anasema watu wakiongelea rushwa Afrika jicho lao ni kwa viongozi tu, lakini ukweli ni kuwa jamii nzima ya Kiafrika wakati mwingine huwa imeoza kwa rushwa. Na anasema dawa si kunyoosheana vidole tu bali kusambaza elimu ya uraia kwa Waafrika ili kuelewa madhara ya rushwa.

Rais anaviasa vyombo vya habari vya nje kutendea haki bara la Afrika katika utoaji wao wa habari. Anasema, kwa mfano, ni kweli Dafur - Sudan kuna matatizo na vyombo vyote vya habari vimetupa jicho pale tu, yani kama vile Dafur ni Afrika yote. Ukweli ni kuwa Afrika ni sehemu tu ya nchi ya Kiafrika na kuna mambo mengi mengine mazuri yanaendelea sehemu nyingine ya Afrika, kwa nini basi vyombo hivi visitangaze habari zote kwa usawa? Watu makofi wawawawa!

Ala! Kumbe amemaliza aisee, ameshasimama na huyo anatoweka zake. Najaribu kupata picha lakini mambo ni yaleyale, jamaa wa usalama ashakaa mbele ya kamera.

Najua unauliza kama nitakwenda kupiga picha na Rais, jibu ni "labda akimaliza kipindi chake cha Urais."

USALAMA WA RAIS KWANZA

Yule rais kipenzi cha Watanzania, namaanisha Kikwete, ambaye muda wote anatabasamu, yani hata kama anakuadhibu tabasamu haling'oki, atakuwa hapa Ngurudoto leo ili kuufunga mkutano wa TED.

Hajafika bado na akitia timu tu (akiwasili) fasta namrusha hapa kwenye blogu. Dah! Ukiwa rais safi sana, yani huguswi, na uwezekano wa wewe kudhuriwa ni mdogo sana. Lazima niwe rais siku moja. Kwa nini nasema hivi? Kwa sababu jinsi jamaa wa usalama wa taifa walivyokuwa wanatukagua leo kabla ya kuingia kwenye ukumbi, mi mwenyewe nikakoma. Manaake inabidi uonyeshe kila ulichonacho kwa usalama wa rais. Nikaanza kuwaza, sasa hawa jamaa si wanaweza wakatuambia tuvue nguo kabisa.

Baadae.

Wednesday, June 6, 2007

KUTANA NA ORY

Ory Okolloh, dada wa Kikenya huyu. Anaishi Cape-Town, Afrika Kusini. Yeye ni mwanablog, mwanasheria na mwanaharakati. Ni mmoja wa watu walionipa msukumo mkubwa wa kuingia kwenye mambo ya blog. Fikiri mtu anakaa nje ya Kenya lakini ukiingia kwenye blogu yake utadhani anakaa Nairobi. Mchango wake ni mkubwa kuliko hata watu wanaokaa Kenya. Tafadhali ungana nami kumshukuru kwa kutembelea blogu yake ya www.kenyanpundit.com

JANE GODALL NA SOKWE WA GOMBE

Jane Godall anatoa mada sasa. Ametusalimia kwa lugha zote yaani Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa, n.k. Lakini kuna hii moja, si mara yangu ya kwanza kumsikia akiitumia, ndio hasa iliyowachota watu hapa mkutanoni. Amesalimia kwa lugha ya sokwe.

Anaongelea mambo mengi kwa kweli, unaweza ukayaona kwenye www.jikomboe.com

Kuna kitu kimoja Jane anauliza, " Ni kwa nini leo binadamu anafanya maamuzi kwa kuangalia tu ni kwa jinsi gani maamuzi hayo yatamuathiri aidha kesho au kesho kutwa wakati babu zetu walikuwa wakifanya maamuzi si kwa kujiangalia wao wenyewe bali vizazi vyao vya baadae.

Alipokuja nchini mwaka 1960 kuanza maisha yake Tanganyika, msitu wa Gombe ulikuwa umenona na kulikuwa na sokwe milioni moja na ushehe sasa iweje leo msitu unakwisha na sokwe wamebaki takribani 150,000 tu. Anatuasa wanaTED kuwa katika kufikiria kwetu kuhusu mustakabali wa Afrika na maendeleo ya kiteknolojia hatuna budi kupigia kelele uharibifu unaosababishwa kwa kisingizio cha maendeleo ya teknolojia.

Kabla ya kutoa mada yake nilikutana na Jane asubuhi wenye chai ya saa nne. Nikaongea nae mambo kadhaa na hatimae nikafanikiwa kupata nilichokua nahitaji. Kumbukumbu, ambayo toka jan nilikua naikimbiza. Asante Jane!

BI. KIDUDE NOMA!



Ni muda wa jionijioni hivi, watu wametoka kunywa chai. Ni zamu ya mkongwe wa muziki wa pwani (Taarabu) kulitifua Jukwaa. Bi Kidude si mchezo aisee. Bibi wa miaka 95, cheki alivolikamatia goma, na sauti inatoka zi mchezo. Kuna hao kina dada nao mhhh! Kwa habari zaidi hebu tembelea www.jikomboe.com

NDESANJO NDANI YA NYUMBA

Ndesanjo amefika juzi usiku. Ile natoka tu kwenye chumba cha mkutano namkuta akisalimiana na watu. Jamaa ni mtu mmoja safi sana. Picha hii nilimpiga jana, muda mfupi kabla Bi. Kidude hajalichakaza jukwaa la TED. Jamaa anablogu sio mchezo. Anaipenda kazi yake. Sasa jana jioni tulipotoka kwenye mkutano ndio akaniongoza katika tohara hii ya kuwa na blogu na hatimaye "Mwenye Macho..." imezaliwa. Asante Ndesanjo, japo jana sikulala hadi saa tisa usiku.

UHURU!

ROKIA ANAKUJA KUGAWA DOZI NYINGINE!

Siku ya kwanza inaelekea ukingoni. Lakini jamaa wa TED hawatuachi hivihivi, wanamrudisha tena Rokia Traore kwenye jukwa. Aisee natamani Ray C na Lady JD wangekuwa hapa wabadilishane mawazo na mtu huyu.

Anakamata gitaa lake sasa, pembeni yake kuna dada mmoja anaonekana kama mwenyeji wa Ethiopia hivi, ni mrembo we acha tu. Napata wasiwasi kidogo, sasa mbona hakuna mpiga drums, kinanda na vingine kama hivyo? Ahh! Kuna jamaa mmoja atapiga kinubi, halafu kuna mwingine ameshikilia kora.

Hebu subiri kwanza, hawa jamaa wanafanya utani, Bendi watu wanne!? Hapana mimi nimeshazoea hapa kwetu bendi watu kuanzia kumi na tano na kuendelea. Sijui, ngoja tusikilize.

Ayayayayaya! Ebwana si mchezo, huyu Rokia anaweza kusimama mwenye jukwaani bila hata kinubi na watu watapiga makofi. Dada anaimba bwana wacha. Kuna huyu jamaa anayepiga kora hapa, anatabasamu mwanzo hadi mwisho. Watu wanapenda kazi zao bwana.

Napiga picha hapa lakini nimekaa kimtegomtego, yani Rokia akishuka tu jukwaani nnae, nitasmile kidogo halafu ntampa, “May I have a photo with you please?”. Nasikia kiingereza hajui sana kwa hiyo hakutakuwa na mabishano marefu. Anatumia zaidi lugha yake ya asili lakini yuko mbali sana kuliko sisi tunaolazimisha lugha za wenzetu.

Nilijaribu kumtafuta Bono ila sijui alipotelea wapi. Jamaa yuko bize sana.

Rokia anamaliza nyimbo zake tatu na watu wanashindwa kubaki vitini, wamesimama kwa dakika kama moja na nusu hivi. Wakati wanaendelea kushangaa na kushangilia mimi najivuta kwa Rokia tayari kupata picha ya ukumbusho. Kumbe je, ntaonyesha nini wajukuu zangu? Tukutane siku ya pili.

MAKAMUZI YANAENDELEA

Tumerudi baada ya mapumziko mafupi. WanaTED bila kupoteza wakati tunampandisha jukwaani mtengeneza filamu wa Kinigeria, lakini anayefanyia kazi zake Ulaya. Huyu anaitwa Newton Aduaka. Alikuwa anakaa London kwanza halafu sasa anakaa Paris. Kama kawaida yangu lazima nitamkamata tu ili nitwange nae "fotografia".

Anasema filamu zake anazotengeneza ni taswira ya maisha yake. Anatuonyesha vipande vifupi vya kazi zake kama nne moja ikiwa ni ile filamu ya "Ezra". Hii ni filamu inayoonyesha jinsi vita ya wenyewe kwa wenyewe ilivyoathiri Waafrika wa pale Sierra Leon. Anatuambia sisi kama Waafrika kabla ya kusonga mbele ni lazima tugeuke nyuma kwanza ili tusijerudia makosa. Filamu hii ilishinda zawadi kubwa ya tamasha la FESPACO pamoja na United Nations Peace Promotion Prize.


Tembelea tovuti yake www.planusa.org

MAPUMZIKO

Duh, sio mchezo Watanzania. Tunapumzika sasa wana TED. Wenye kupata chai wakapate chai, wenye kupata kahawa wakapate na wenye kwenda kujistiri wakajistiri.

Mimi nazungukazunguka kutengeneza mtandao. Kwani nini maana ya mikutano? Ukienda kwenye mkutano halafu usitengeneze rafiki hata mmoja ujue mkutano umekushinda. Nzungukazunguka na nnakutana na Salim Amin, huyu ni mtoto wa Moh'd Amini, yule mwanahabari na mtengeneza filamu aliyeweka ukweli wa baa la njaa kule Ethiopia mwaka 1985. Salim amenichekesha sana, ananiambia baba yake walifanya kazi pamoja na Rais wetu msataafu miaka ile na baba yake alikuwa akimpa Mkapa lifti kweye skuta kila asubuhi.

Pia napata picha ya kumbukumbu na rafiki yangu David McQueen. Mwingereza huyu. Jamaa kila saa anaongelea jinsi anayomiss mkewe. Kula leki walai!

Kupumzika hakuna maana ya kulala ewe mwafrika, tengeneza mtandao kwani utandawazi uko mlangoni mwako! Tukutane ukumbini kwa ungwe ya pili.

MISAADA YA WLIOENDELEA NI UPPUZI KWA MWAFRIKA

Huyu ni Andrew Mwenda, mwandishi wa habari na mtaalamu wa masuala ya jamii toka Uganda.
Jamaa ana mzuka balaa. Anawashambulia wazungu wanaoleta misaada kwa waafrika bila kufanya tathmini kuwa misaada hiyo inamsaidia nani.

Ayayayayaya! Jamaa anaenda mbele zaidi na kuzipiga shuti serikali za kiafrika kuwa hazijafanya chochote kwa kupitia misaada. Anasema misaada inawalemaza waafrika.
Anaiuliza hadhira sasa iwapo kuna yoyote anayefahamu nchi iliyoendelea kwa kupewa misaada. Watu kimyaaaaa! Halafu ghafla kuna mtu ananyoosha mkono, uliza ni nani? Bono, yule mwanamuziki maarufu wa Rock ambaye amevalia njuga kwelikweli vita dhidi ya umasikini Afrika. Yuko hapa, alitakiwa awe kwenye mkutano wa G8 ila amewatoroka.

Bono anapatiwa nafasi ya kuongea na kuitolea mfano nchi yake ya uzaliwa, Northern Ireland kuwa ni nchi mmoja wapo amabyo imetumia misaada kuisimama kwa miguu yake mwenyewe.

Wanabishana na mwenda lakini baada ya mkutano wanakaa pamoja na kupata mvinyo. Wanakubaliana kutokubaliana. Kula leki TED!

AFRIKA I TAYARI KWA BIASHARA.

Jukwaani yupo Carol Pineau. Yeye ni mwandishi wa Habari na mtengeneza filamu. Huyu yeye ameshatengeneza filamu kwenye maeneo yenye vita, njaa na migogoro mingine inayohusu Afrika hadi pale alipoamua "kuzaliwa upya" yani kutafuta mada chanya kwa ajili ya filamu zake. Sasa amegundua kuwa Afrika ina habari zingine pia na si matatizo tu. Filamu yake ya "Africa Open for Business" imempatia heshima kubwa sana ulimwenguni kote.

Kwa maneno yake mwenye akizungumzia filamu yake hiyo anasema, "It shows enterpreneurs in the one place no one expected to find them, Africa". Kweli hii ni Africa the next chapter.

Tafadhali tembelea tovuti yake, www.africaopenforbusiness.com. Hapa anatuonyesha sehemu ya filamu yake mpya itakayoitwa "Africa Investment Horizon".

HAPA NI DOZI JUU YA DOZI

Rokia amemaliza kutukaribisha, ameimba kwa lugha moja wapo ya kule kwao Mali. Wengi hatujaelewa neno kwa neno kwa kile alichoimba lakini kwa uelewa wa jumla amtukaribisha Afrika.

Inapita kama dakika moja na nusu halafu kwenye jukwaa anakaribishwa mwongozaji wa sinema na mpiga picha wa siku nyingi, bwana Andrew Dosunmu, yeye anatoka Nigeria. Ameshaongoza filamu ya "Hot Irons" (1999), ameongoza pia mchezo wa luninga huko Afrika ya Kusini uitwao "Yizo-Yizo". Ila katika kazi zote za huyu jamaa iko moja amabyo imenimaliza kabisa, yeye ndiye aliyetengeneza video ya muziki wa "Birima" wa Yossou N'dour. N'dour naye ilikuwa awepo hapa leo lakini ana shughuli za kibinafsi.
Dosunmu anasema wapiga picha na watengeneza filamu wa kiafrika tunawajibika kuonyesha upande wa pili wa maisha ya mwafrika kwa mtazamo wetu wenyewe, CNN na BBC na FOX TV hawalazimiki kufanya hivyo kwani kwao habari mbaya kuhusu Afrika ndiyo inayouza. Duh! Jamaa anaongea ile pidgin ya Kinigeria, simpati kila neno.

Nashindwa kujizuia, namsaka Dosunmu na kupiga naye picha. Tafadhali tembelea tovuti yake ya www.andrewdosunmu.com ujionee kazi zake.

Tuesday, June 5, 2007

MCHAKAMCHAKA UNAANZA

Usifanye mchezo aisee, jamaa wa stage design ni kiboko. Huu ukumbi ukiingia humu unasahau kabisa kwamba kuna shida duniani. Jamaa wako kamili kila kitu kuanzia lighting, sound na mazagazaga yote. Ila duh! nasikia jamaa wa TED wamewaleta kutoka Afrika ya kusini. Hivi kwani Rita Paulsen na Benchmark yake si huwa wanafanya hizi kazi, sasa alikuwa wapi hakuchangamkia tenda hii atutoe Watanzania kimasomaso.

Aisee binadamu ni watu wa ajabu sana, katika zoezi la kuingia humu ndani hata watu wazima kabisa wanagombea nafasi za mbele. Si unajua tena. Na mimi nikiwemo :-)
Aisee nyie, hebu ngojeni kwanza! Otea ni nani anayeuanzisha mchakamchaka huu wa TED, aisee siamini, yani kwa macho yangu, kwa maana nyingine "live" namwona Rokia Traore stejini. Kama hujawahi kumsikia Rokia basi hujapata sikiliza muziki wa Kiafrika Magharibi wewe.

LAZIMA NIPIGE NAE PICHA, ROKIA WEEEEE! Kamua mama.

DUH!

Aisee ni noma, mkutano bado dakika kadhaa uanze, yule mwanablogu mtukutu, Ndesanjo Macha hajatia timu. Ndesanjooooo! unaua bendi babuu. Niliposoma blogu yake siku ya tarehe 2 Juni kwamba jamaa wamemletea maroroso uwanja wa ndege huko ughaibuni hadi kusababisha jamaa kuikosa ndege nikajua anatania, si unajua wabongo kwa kupigana fix sometimes.

Haina noma sana lakini kwani ametuhakikishia kuwa hata kama ni kuikosa TED basi itakuwa kwa siku hii ya kwanza tu.

Watu ni lukuki hapa. Na kila mtu anaongea lugha fulani ambayo kwa namna fulani inahusihwa na tarakilishi (kompyuta), usipime mjomba.

Ahh! Hata Jane Godoll yupo. Nataka sana nipige nae picha aisee ila kila nikijisogeza kuna mtu anamuwahi. Bibi maarufu sana huyu. Atatoa mada kesho kuhusu sokwe na nyumba yao inayotoweka (msitu)

UTANDAWAZI SOO!


Mkutano wa TED unafurahisha sana, nakaa natafakari kuwa sisi Watanzania tunaupokeaje utandawazi.

Hawa jamaa wako kwenye mgahawa wa Internet hapa Ngurudoto, Arusha, wanawasiliana na ulimwengu wote. Yani wanaupasha habari ulimwengu juu ya kile kinachoendelea hapa sasa. Kuna huyo dada hapo kushoto, ni rafiki yangu anaitwa Jen Brea, yeye ni mpiga picha pia. Tulikutana mtandaoni halafu tumekutana kwa mara yay kwanza "live" hapa Arusha. Yeye ni Mmarekani lakini anakaa Beijing, China. Nafikiri anawaandikia rafiki zake huko. Mcheki kwenye www.jenbrea.net

Kuna huyo bwana mweusi hapo kulia, yeye anaitwa David McQueen. Ni mwingereza. Yeye ni mtaalamu wa kufundisha watu kuzungumza mbele ya hadhira. Kama una tatizo la kuikabili hadhira mtafute jamaa fasta kwenye www.milestoneunltd.com. Jamaa anasema ana uzoefu wa kufundisha kwa miaka 20 sasa. Nilimfuma anachat na mkewe, anamwambia "Arusha safi sana!"

Hao wachina watatu sina habari zao ila nao wako kwenye TED.
Utandawazi unakutanisha jamii zote hata ubishe vipi.

TED HIYO!


Hapa ni hoteli ya Ngurudoto, jijini Arusha. Mkutano wa TED unafanyika hapa kwa mara ya kwanza Afrika. Mkutano huu unajumuisha watu wa kila rangi toka mabara yote hapa ulimwenguni ambamo watu wanaishi. Mkutano una dhumuni la kukutanisha wanaharakati wa teknologia digitali, wasanii wanaotumia teknolojia digitali, na wabunifu wanaotumia teknologia hiyo. Mimi nahudhuria kama mtengeneza filamu na mpiga picha wa kujitegemea. Mkutano huu umepewa jina la "Africa the Next Chapter". Mkutano huu umeanza tarehe 4/6 na utadumu kwa siku nne.

KARIBU KWA MWENYE MACHO...



Karibu kwenye blogu ya Mwenye Macho... Blogu hii itakuwa ni ya picha zaidi kuliko maneno. Naitwa Babukadja Sankofa Msangi(ama kwa jina la zamani Philemon). Kwa bahati iliyo njema blogu hii inazaliwa siku moja baada ya kuanza kwa mkutano mkubwa wa maswala ya teknolojia, burudani na ubunifu yani TED. Nafurahi kukuletea habari za mkutano huu kwa njia ya picha. KARIBU!