Tuesday, June 5, 2007

DUH!

Aisee ni noma, mkutano bado dakika kadhaa uanze, yule mwanablogu mtukutu, Ndesanjo Macha hajatia timu. Ndesanjooooo! unaua bendi babuu. Niliposoma blogu yake siku ya tarehe 2 Juni kwamba jamaa wamemletea maroroso uwanja wa ndege huko ughaibuni hadi kusababisha jamaa kuikosa ndege nikajua anatania, si unajua wabongo kwa kupigana fix sometimes.

Haina noma sana lakini kwani ametuhakikishia kuwa hata kama ni kuikosa TED basi itakuwa kwa siku hii ya kwanza tu.

Watu ni lukuki hapa. Na kila mtu anaongea lugha fulani ambayo kwa namna fulani inahusihwa na tarakilishi (kompyuta), usipime mjomba.

Ahh! Hata Jane Godoll yupo. Nataka sana nipige nae picha aisee ila kila nikijisogeza kuna mtu anamuwahi. Bibi maarufu sana huyu. Atatoa mada kesho kuhusu sokwe na nyumba yao inayotoweka (msitu)

UTANDAWAZI SOO!


Mkutano wa TED unafurahisha sana, nakaa natafakari kuwa sisi Watanzania tunaupokeaje utandawazi.

Hawa jamaa wako kwenye mgahawa wa Internet hapa Ngurudoto, Arusha, wanawasiliana na ulimwengu wote. Yani wanaupasha habari ulimwengu juu ya kile kinachoendelea hapa sasa. Kuna huyo dada hapo kushoto, ni rafiki yangu anaitwa Jen Brea, yeye ni mpiga picha pia. Tulikutana mtandaoni halafu tumekutana kwa mara yay kwanza "live" hapa Arusha. Yeye ni Mmarekani lakini anakaa Beijing, China. Nafikiri anawaandikia rafiki zake huko. Mcheki kwenye www.jenbrea.net

Kuna huyo bwana mweusi hapo kulia, yeye anaitwa David McQueen. Ni mwingereza. Yeye ni mtaalamu wa kufundisha watu kuzungumza mbele ya hadhira. Kama una tatizo la kuikabili hadhira mtafute jamaa fasta kwenye www.milestoneunltd.com. Jamaa anasema ana uzoefu wa kufundisha kwa miaka 20 sasa. Nilimfuma anachat na mkewe, anamwambia "Arusha safi sana!"

Hao wachina watatu sina habari zao ila nao wako kwenye TED.
Utandawazi unakutanisha jamii zote hata ubishe vipi.

TED HIYO!


Hapa ni hoteli ya Ngurudoto, jijini Arusha. Mkutano wa TED unafanyika hapa kwa mara ya kwanza Afrika. Mkutano huu unajumuisha watu wa kila rangi toka mabara yote hapa ulimwenguni ambamo watu wanaishi. Mkutano una dhumuni la kukutanisha wanaharakati wa teknologia digitali, wasanii wanaotumia teknolojia digitali, na wabunifu wanaotumia teknologia hiyo. Mimi nahudhuria kama mtengeneza filamu na mpiga picha wa kujitegemea. Mkutano huu umepewa jina la "Africa the Next Chapter". Mkutano huu umeanza tarehe 4/6 na utadumu kwa siku nne.

KARIBU KWA MWENYE MACHO...



Karibu kwenye blogu ya Mwenye Macho... Blogu hii itakuwa ni ya picha zaidi kuliko maneno. Naitwa Babukadja Sankofa Msangi(ama kwa jina la zamani Philemon). Kwa bahati iliyo njema blogu hii inazaliwa siku moja baada ya kuanza kwa mkutano mkubwa wa maswala ya teknolojia, burudani na ubunifu yani TED. Nafurahi kukuletea habari za mkutano huu kwa njia ya picha. KARIBU!