Thursday, July 12, 2007

TUMAINI!

Mara Ngapi umesikia vilio toka Gaza?

Mara ngapi umesikia wazazi wa Kimarekani wanaolilia watoto wao waliopelekwa na Joji 'Kichaka' huko Iraq wakiwa hawana matumaini ya kurejea tena?

Mara ngapi umesikia kuhusu kilichotokea Rwanda, na sasa kinatokea tena Dafur na halafu wote tukajifanya kutokuwa na habari?

Mara ngapi umesikia kuhusu Robert Mugabe akiua watu wake kwa kisingizio cha kuwakomesha 'mabwana' wakubwa wa Magharibi?

Mara ngapi umesikia mwanasiasa wako akikupa ahadi za maisha matamu, kisha akajituniku mwenyewe?

Tazama,

Kungali na giza totoro sitakoma kuingoja nuru

Mjumbe atarejea tena.

Tumaini litarejea tena.

Monday, July 9, 2007

SERIKALI YA BONGO NA BAJETI YA 2007/2008

Wakati wa kampeni za urais wa Tanzania mwaka 2005, Rais wa sasa alikuwa na msemo wake maarufu wa "Maisha bora kwa kila Mtanzania". Msemo ule niliufananisha na sahani hizi nzuri na mavijiko yake makubwa yanayoashiria kuwa mlo baada ya jamaa kuingia madarakani ungekuwa babkubwa.

Salaaalah, kumbe baba mwenye nyumba (Rais Kikwete) alikuwa akituahidi watoto wake (Watanzania) kwamba tutakula pilau na nyama ya kubanika (maisha bora) pasipo kuwasiliana na mpishi mkuu (Waziri wa Fedha, Mh. Zakhia Meghji) na kupata uhakika iwapo kiroba cha mchele, fungu la nyama, vitunguu na mafuta yapo.

Basi tumekabidhiwa sahani hizi na mavijiko haya (Ahadi hewa) tangu mwaka 2005 lakini chakula (maisha bora kwa kila mtanzania) bado havijaja na havitakuja karibuni. Sasa watoto (Watanzania) tumeanza kuvuta suruali ya baba (Rais Kikwete) kuuliza kulikoni, baba hana jibu anamuuliza mpishi mkuu (Mh. Meghji) kulikoni, mpishi mkuu anatukunjia ndita watoto (Watanzania na Vyombo vya habari vya ndani) eti tunamchonganisha na baba.

Mpishi mkuu anatoa jibu la haraka haraka, ili kulinda unga wake. Anasema, "Subirini dakika tano jamani (yani baada ya miaka mitano)". Watoto tunakuja juu, kaka zetu (Vyombo vya habari) wanaenda mbele zaidi na kumvuta mpishi mkuu nywele. Mpishi mkuu anawauliza kina kaka "Uko wapi uvumilivu wenu (yani uko wapi uzalendo wenu), mbona ndugu zenu wa kambo (Vyombo vya habari vya nje) wanaweza kuvumilia, nyie mna njaa ya kiasi gani?"

Ukweli ni kuwa bajeti ya Bongo mwaka huu ni ya kufunga mikanda japo Mh. Meghji anakana hilo. Je Tuanze kulia kama wana wa Israel walipomlilia Musa wakidai kurudi utumwani Misri wakaendelee kula nyama wangali wakichapwa mijeledi mgongoni?

Picha hii nimeipiga kwenye kongamano fulani kule Msasani juma lililopita.

Tuesday, July 3, 2007

MWENYE MACHO AUZA PICHA YA KWANZA

Hatimaye Mwenye Macho ameuza picha yake ya kwanza katika maisha yake ya upigaji picha kwenye jarida moja huko Ufaransa kupitia wakala wa picha aitwaye Cedric Galbe. Cedric Galbe ni mpiga wa Kifaransa ambaye ameanzisha tovuti iitwayo http://www.galbe.com/. Tovuti hii ni wakala wa wapiga picha toka Africa, Scandinavia, Mashariki ya Kati, na Marekani ya Kusini.

Picha aliyouza ni hiyo hapo juu ya mtaalamu wa hesabu aitwaye Ron. Ron alitoa mada kwenye mkutano wa TED uliofanyika Arusha mwezi uliopita. Mada yake ilikuwa inaonyesha ni kwa jinsi gani hesabu zinavyothibitisha kuwa maisha yalianzia Afrika. Kwa habari zake zaidi tembelea http://www.jikomboe.com/, Ndesanjo alimwandika vizuri zaidi. Mimi sikumwelewa sawasawa kwani mimi na hesabu hatukuwahi kuwa marafiki hata kidogo.

Mpaka wakati mwingine, naelekea benki mara moja kuona kama dola zangu zimeingia.

Sunday, July 1, 2007

KUNA UTAMADUNI MPYA NYUMBANI

Unamkumbuka Rhymson, mmoja wa waasisi wa Hip Hop hapa Tanzania? Alikuwa na kundi la mwanzo kabisa la mtindo huo wa muziki, likiitwa KWANZA UNITY. Siku hizi Rhymson ni mwafrika aliyezaliwa upya na anaitwa Zavara.

Zavara alikuwa ughaibuni kwa takribani miaka isiyopungua kumi, huko Kanada na Marikani. Huko alikuwa akifanya shughuli za mziki pamoja na filamu. Sasa baada ya kipindi chote hicho amerejea hapa nyumbani na kuungana na "Waafrika" wa hapa ili kuweza kupeleka jahazi la mziki wa Hip Hop mbele, katika mstari ulionyooka.

Zavara pamoja na "Waafrika" kadhaa wa hapa akiwemo msanii na mwanaharakti aitwaye Mejah wameungana na kuanzisha mradi uitwao "Uma Project". Huu ni mradi wenye lengo la kukusanya vijana wa "Kiafrika" wenye ndoto ya kufanikiwa katika sanaa bila kuisahau asili yao. Vijana hawa wengi wao ni wale wasio na uwezo wa kifedha kuweza kufanikisha ndoto zao.

Uma Project huandaa tamasha kila jumamosi ya mwisho wa mwezi na kuwakutanisha vijana pale British Council, Dar es Salaam. Sasa jana lilikuwa ni tamasha la tatu na lilipewa jina la "WEWE NI NANI?". Jina hili lina dhumuni la kumfanya kila binadamu kujiuliza kuhusu uwepo wake kabla hujafanya jambo na kuhakikisha iwapo unajitambua. Tamasha la mwezi uliopita liliitwa "USWAZI WAPI?".

Katika tamasha la jana kulikuwa kuna wachoraji, wanamuziki, wapiga picha mgando na za video, watu wa masuala ya mitindo ya mavazi (Wakiongozwa na Merinyo wa Afrika sana), na wengine wengi.

Kila kitu kilikuwa poa sana ila nilivutiwa sana na sanaa ya kuchora grafiti ukutani. Sanaa hii inasimamiwa na kuongozwa na Mejah, yeye ni mtaalamu wa sanaa hii, aliisomea kule New York, Marikani. British Council wamejitolea ukuta ambao vijana wa kitanzania wanapatiwa fursa ya kuandika grafiti kuelezea hisia na mawazo yao. Picha hizi za grafiti hudumu kwa muda wa mwezi mmoja halafu hufutwa na kuta kupakwa rangi nyeupe tayari kwa watu kuchora tena katika tamasha linalofuata.

Elimu ya Grafiti hutolewa bure pale, rangi pia hutolewa bure na jamaa wa British Council. Kwa kweli huu ni utamaduni mpya hapa nyumbani, na ni kitu poa sana kwani unawafanya vijana wa kiafrika kujitambua katika kila wanachijatahidi kufanya.