Monday, July 9, 2007

SERIKALI YA BONGO NA BAJETI YA 2007/2008

Wakati wa kampeni za urais wa Tanzania mwaka 2005, Rais wa sasa alikuwa na msemo wake maarufu wa "Maisha bora kwa kila Mtanzania". Msemo ule niliufananisha na sahani hizi nzuri na mavijiko yake makubwa yanayoashiria kuwa mlo baada ya jamaa kuingia madarakani ungekuwa babkubwa.

Salaaalah, kumbe baba mwenye nyumba (Rais Kikwete) alikuwa akituahidi watoto wake (Watanzania) kwamba tutakula pilau na nyama ya kubanika (maisha bora) pasipo kuwasiliana na mpishi mkuu (Waziri wa Fedha, Mh. Zakhia Meghji) na kupata uhakika iwapo kiroba cha mchele, fungu la nyama, vitunguu na mafuta yapo.

Basi tumekabidhiwa sahani hizi na mavijiko haya (Ahadi hewa) tangu mwaka 2005 lakini chakula (maisha bora kwa kila mtanzania) bado havijaja na havitakuja karibuni. Sasa watoto (Watanzania) tumeanza kuvuta suruali ya baba (Rais Kikwete) kuuliza kulikoni, baba hana jibu anamuuliza mpishi mkuu (Mh. Meghji) kulikoni, mpishi mkuu anatukunjia ndita watoto (Watanzania na Vyombo vya habari vya ndani) eti tunamchonganisha na baba.

Mpishi mkuu anatoa jibu la haraka haraka, ili kulinda unga wake. Anasema, "Subirini dakika tano jamani (yani baada ya miaka mitano)". Watoto tunakuja juu, kaka zetu (Vyombo vya habari) wanaenda mbele zaidi na kumvuta mpishi mkuu nywele. Mpishi mkuu anawauliza kina kaka "Uko wapi uvumilivu wenu (yani uko wapi uzalendo wenu), mbona ndugu zenu wa kambo (Vyombo vya habari vya nje) wanaweza kuvumilia, nyie mna njaa ya kiasi gani?"

Ukweli ni kuwa bajeti ya Bongo mwaka huu ni ya kufunga mikanda japo Mh. Meghji anakana hilo. Je Tuanze kulia kama wana wa Israel walipomlilia Musa wakidai kurudi utumwani Misri wakaendelee kula nyama wangali wakichapwa mijeledi mgongoni?

Picha hii nimeipiga kwenye kongamano fulani kule Msasani juma lililopita.

No comments: