Monday, June 11, 2007

HONGERA SUMAYE LAKINI...!

Basi tangu nimetoka kwenye mkutano wa TED nimekuwa na mambo kadhaa yananikimbiza mchakamchaka hadi muda wa kublog unataka kuniponyoka. Lakini nimejiwekea nadhiri kuwa japo mara moja kwa wiki lazima nipandishe kitu hapa.

Sasa leo katika upekuzi wangu nikagonga hodi www.mjengwa.blogspot.com. Ile kukaribishwa tu nikakutana na picha hii. Sikuwa na lazaidi la kusema zaidi ya kumpongeza Sumaye.


Lakini wakati huohuo nikaanza kuwaza, unajua jamaa alipokuwa Waziri "Mkubwa" tulikuwa tunampa heshima kama Mungu. Kwa mfano tulikuwa tukitaka kumwambia jambo lazima uanze na "Mheshimiwa Waziri 'Mkubwa'...", halafu ndio unaendelea na swala lako unalotaka kusema, labda, "Mheshimiwa Waziri 'Mkubwa', samahani naweza kukuvua viatu". Sasa nikawa najiuliza jamaa si atakuwa amepata tabu sana pale Havard maana huko nasikia walikuwa wanampita tu, wale wachache waliokuwa wanaomfahamu ndio labda walikuwa wakimwita kwa jina lake la kwanza, mfano, "Freddy ehh, unajua kesho ndio 'deadline' ya 'assignment', mbona jana hatukukuona kwenye 'discussion'?".


Mbili, jamaa alipokuwa kiongozi hapa yani hata hotuba ya karatasi mbili alikuwa anabebewa. Kula leki viongozi wa kibongo! Sasa huko sijui nani alikuwa anambebea majitabu yake, labda aliajiri mtu!


Tatu, niliposikia jamaa anakwenda kusomea uongozi nikapigwa na butwaa na maswali kibao yakajiri kichwani mwangu. Swali kubwa lilikuwa ni "Umetuongozaje kwa miaka kumi bila ya kuwa na ujuzi wa kuongoza?" Hata hivyo nikajifariji kuwa labda sasa baada ya kuhitimu Freddy atakuwa anajua kuwa kiongozi aliye bora sio tu habebewi hotuba, bali hata kuandikiwa ni mwiko, kwani mbebaji anaweza kupoteza baadhi ya kurasa na mwandishi huandika mawazo yake na siyo ya mtoa hotuba.


Sina la ziada zaidi ya kumpongeza aliyekuwa Waziri 'Mkubwa' wetu, HONGERA FREDDY!

No comments: