Friday, June 8, 2007

YALIYOJIRI JANA

Najitayarisha kwenda uwanja wa ndege wa Kilimamanjaro tayari kurudi nyumbani. Lakini kuna vitu nilitakiwa kuvirusha jana ila muda ukabana. Naona haitakuwa vyema kuondoka bila kukupatia.

Jana jioni baada ya mapumziko mafupi, na chai ya jioni, kwenye jukwaa alipanda Chris Abani. Yeye ni Mwandishi wa vitabu na mshairi. Ababni ni Mnigeria kalini anakaa Marekani, ni profesa wa masuala ya fasihi katika chuo kikuu kule.

Abani ameandika mambo mengi ya kukosoa unyonyaji wa bara la Afrika na pia amekuwa mwiba mchungu kwa viongozi maharamia wa Nigeria na Afirka pia. Amewahi kufungwa jela mara tatu kwa sababu ya maandishi na mashairi yake yasiyo na sime kusema "MFALME YUKO UCHI!"

Abani amepanda kwenye jukwaa na anongelea jinsi teknolojia inavyomsaidi kuandika mambo ya nyumbani angali yu mbali. Anaongea mambo kadhaa tafadhali yasome kwa Ethan Zuckerman na Ndesanjo Macha.

Ababni anamaliza dakika zake arobaini na tano alizopewa kutoa mada, lakini hatuachi hivihivi anatuacha na Shairi. Anapomaliza ukumbi unalipuka kwa vigelegele na vifijo. Aisee huyu jamaa si mchezo.

Kabla hata hatujajiweka vyema kwenye viti vyetu, unapanda mwiba mwingine wa uandishi toka Kenya, huyu si mwingine bali Binyavanga Wainaina. Sitaki kukuficha, huyu jamaa sijawahi kumwelewa hata siku moja, huwa anaongea mambo mengi kwa wakati mmoja. Mara ya kwanza nilikutana naye Zanziba mwaka 2005, kwenye tamasha la filamu, akanizawadia insha yake iitwayo "How to Write About Africa". Ilinibidi kuisoma mara tatu kuweza kuelewa alichokuwa anasema.

Sasa leo tena amepanda hapa jukwaani na kutuambia tufunge macho. Halafu anaanza kusoma insha yake fulani hivi, kwa dakika mbili. Anapotuambia tufungue macho watu kadhaa wanapiga makofi ila nina hakika wengi wetu, mimi nikiwemo tunafuata mkumbo tu, hatujaelewa kitu. Binyavanga anatabasamu kwa sababu anajua ameshawakoroga watu, anashukuru na kuondoka zake. Soma zaidi kuhusu Binyavanga katika www.jikomboe.com

Baadae jukwaani anapanda Franco Sacchi, ni mtengeneza filamu na Prodyusa wa filamu ya This is Nollywood. Ni Muitaliano huyu jamaa lakini amezaliwa Zambia. Filamu yake ni dokyumentari inayoonyesha maendelea ya utengenezaji wa filamu wa Nigeria. Franco anatwambia kuwa Afrika ikipatiwa Teknolojia muafaka inaweza kwenda sambamba na sehemu zingine za ulimwengu na hili limethibitishwa na maendeeo ya haraka ya fani ya filamu katika Nigeri. Anasema kwa mwaka jana pekee, Nigeria imetengeneza filamu 2000. Nigeria ni nchi ya tatu kwa utengenezaji wa filamu ukiacha Marekani na India.

Franco ameambatana na muongozaji wa filamu za Kinigeria anaitwa Bon Emeruwa, bila ajizi baada ya Franco kumalaiza mada najivuta kukutana na Bond. Kujivuta huku si kwa ajili ya kupata picha tu, hapa ni biashara sasa. Ukumbuke kuwa mimi pia ni mtengeneza filamu. Naongea mambo kadhaa na Bond kama bajeti za filamu zake, anapiga picha kwa muda wa siku ngapi na anasambaza vipi filamu zake. Tunabadilishana anuani zetu, na tunapeana ahadi za kutembeleana na kusaidiana katika miradi ya filamu zetu. Na mwisho namuomba tupige picha ya ukumbusho. Nakuona unatasamu, ahahahahah!

Haya na mwisho kabisa anapanda yule gwiji la muziki toka Afrika ya kusini, yeye anaitwa Vusi Mahlasela. Vusi si mwanamuziki tu, ni mshairi, na alikuwa pia na bado ni wanaharakati dhidi ya ubaguzi wowote wanrangi.

Jamaa anapiga gita lake na kuimba mwenyewe, ila kama uko nje ya ukumbi huu unaweza kudhani kuna watu watatu au wanne kwenye jukwaa. Jamaa kuna namna anashirikiana na gitaa lake na kutoa saiti zaidi ya moja kwa wakati mmoja.

Naona hata Rokia na Abenaa wametulia kimya, bwana mkubwa yuko kazini. Usipime. Soma zaidi kwenye www.jikomboe.com

Hivyo ndivyo kamera yangu ilivyoishuhudia jana.

No comments: