Thursday, June 7, 2007

KILA KITU NI MUHIMU KWANGU - JK

Rais wangu, Kikwete ameshaingia kuufunga mkutano wa TED, dah! yani leo humu ndani hakuna amani kabisa, kumejaa jamaa wa usalama wa taifa kibao na si unajua kuwa wale jamaa huwa hawaruhusiwi kukaa, basi hata picha hatuzipati vizuri. Yani kila nikipata angle nzuri, jamaa kakatiza. Si mbaya lakini, hii ni kwa usalama wa rais wangu.

Sasa mheshimiwa rais anatoa hotuba, wakati anapanda kwenye jukwaa alikuwa amevaa suti yake safi sana. Lakini ili uwe mwanaTED mzuri, amri ya kwanza ni kutokuvaa suti, unatakiwa uvae kawaida ili uweze kufanya kazi. Basi raisi alipopanda tu jukwaani akijistukia kuwa amechemka, fasta akamwita mlinzi wake na kumkabidhi koti, watu full makofi. Ila naona kiongozi wa msafara amekasirika kwa sababu hata yeye amevaa suti, sasa anajishauri, je avue au abaki alivyo? Bosi wake amevua!

JK amenifuraisha kitu kimoja, anazungumzia maendeleo ya Teknolojia na Afrika. Anasema kila kona ya dunia anayokwenda huulizwa ni kitu gani anachotilia umuhimu katika maendeleo ya wananchi wake? Yeye huwajibu "Kila kitu". Hotuba yake ni fupi sana na amemaliza.

Sasa ni kipindi cha maswali, wanaTED wanamuuliza ni kitu gani kinamkera katika siasa za Afrika. Anajibu, "Nafadhaishwa na viongozi wa kijeshi wanaoamka asubuhi moja na kuteka radio na kutangaza serikali mpya isiyo ya kidemokrasia."

Anaulizwa, "Je wewe unajali demokrasia?", kama kawaida yake anatabasamu kwanza halafu anajibu kuwa anadhani anajali demokrasia. Jamaa anauliza unatumia kipimo gani kujua kuwa unajali demokrasia? Anasema, nguzo kubwa anayotumia kujipimia ni uhuru wa vyombo vya habari. Anasema kuna magazeti lukuki Tanzania, na hicho ni kitu kizuri kwani inasaidia kukosoa yule anayetenda kosa na ni jukumu la mkoslewaji kuelewa. Watu makofi wawawawawa!

Anaulizwa, unadhani misaada ni sumu kwa Afrika? Anasema yeye yuko tofauti kabisa na hilo, yeye anaamini kuwa misaada ni kitu safi sana ila itumike vizuri la sivyo itageuka kitanzi kwa mkopaji.

Anazungumzia rushwa Afrika. Anasema watu wakiongelea rushwa Afrika jicho lao ni kwa viongozi tu, lakini ukweli ni kuwa jamii nzima ya Kiafrika wakati mwingine huwa imeoza kwa rushwa. Na anasema dawa si kunyoosheana vidole tu bali kusambaza elimu ya uraia kwa Waafrika ili kuelewa madhara ya rushwa.

Rais anaviasa vyombo vya habari vya nje kutendea haki bara la Afrika katika utoaji wao wa habari. Anasema, kwa mfano, ni kweli Dafur - Sudan kuna matatizo na vyombo vyote vya habari vimetupa jicho pale tu, yani kama vile Dafur ni Afrika yote. Ukweli ni kuwa Afrika ni sehemu tu ya nchi ya Kiafrika na kuna mambo mengi mengine mazuri yanaendelea sehemu nyingine ya Afrika, kwa nini basi vyombo hivi visitangaze habari zote kwa usawa? Watu makofi wawawawa!

Ala! Kumbe amemaliza aisee, ameshasimama na huyo anatoweka zake. Najaribu kupata picha lakini mambo ni yaleyale, jamaa wa usalama ashakaa mbele ya kamera.

Najua unauliza kama nitakwenda kupiga picha na Rais, jibu ni "labda akimaliza kipindi chake cha Urais."

2 comments:

luihamu said...

Mkuu,nimefurahishwa na kazi yako nzuri,ni vyema tukizidi kufahamiana pili tembelea blogu yangu.

haujachelewa kuchukuwa fomu na kuwania uongozi katika jumuiya ya wanablogu Tanzania.

Nuff Nuff Respect man.

Jeff Msangi said...

Kazi nzuri Sankofa.Nimefurahi sana kuona umeingia kwa kishindo katika ulimwengu huu wa blog.Kila la kheri,amani.Tunakumbukana?